Viongozi wa Yanga, juzi Jumamosi waligoma kuwaruhusu wachezaji wao kuingia katika vyumba vya kubadilishia nguo kwenye Uwanja wa Samora mjini Iringa ambapo timu hiyo ilipambana na Lipuli FC.
Sababu kubwa ya viongozi hao kuwazuia wachezaji wao kuingia kati vyumba hivyo ni kile walichodai kuwa kimepuliziwa dawa za kuwapunguza nguvu.
Jambo hilo lilizua mvutano mkubwa baina ya viongozi hao na wale wa Lipuli ambao walikuwa wakiwataka wawaruhusu wachezaji wao waingie vyumbani humo wakidai hiyo ni dawa ya mbu, jambo ambalo halikufanikiwa.
Viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) waliokuwa uwanjani hapo walishindwa kutoa maamuzi yao mara baada ya kwenda kukagua vyumba hivyo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Hussein Nyika, alisema kuwa hata kama ni dawa ya mbu ndiyo iliyokuwa imepuliziwa vyumbani humo wasingeweza kuwaruhusu wachezaji wao kuingia na bora wapigwe faini lakini siyo kuwaangamiza wachezaji wao.
"Hujuma kama hizi siyo za kiungwana kwa hiyo kama TFF watatupiga faini sawa lakini itakuwa ni ya uonevu kwani hata wao wamejionea hilo.
"Kama ni dawa ya mbu kwa nini wasipulizie siku nyingine mpaka wapulizie leo?" alihoji Nyika.
SOURCE: CHAMPIONI
No comments:
Post a Comment