Pamoja na Mbao FC kuwa wamejiandaa na kupania lazima washinde mechi yao leo dhidi ya Yanga, mabingwa hao wanasema wako tayari kwa kazi ya leo.
Yanga tayari iko jijini Mwanza kwa ajili ya mechi hiyo itakayochezwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba.
Kocha Msaidizi wa Yanga, Shadrack Nsajigwa amesema wamejiandaa vizuri na wako tayari kwa mchezo.
“Tumefanya maandalizi yetu vizuri na baadhi ya wachezaji waliokuwa majeruhi wamerudi tena.
“Tunajua Mbao FC ni timu nzuri, lakini tuna kikosi bora na kipo tayari,” alisema.
Yanga ilitua Mwanza kwa ndege tayari kwa ajili ya mechi hiyo ambayo inasubiriwa kwa hamu jijini Dar es Salaam.
Katika msimamo, Yanga iko katika nafasi ya tatu na inataka kushinda mechi hiyo ili kujiweka sawa ingawa hata ikishinda itaendelea kubaki katika nafasi ya tatu.
Simba ndiyo vinara wakiwa na pointi 26 sawa na Azam FC walio katika nafasi ya pili wakati Yanga wana pointi 21 na lazima washinde ili kupunguza pengo.
No comments:
Post a Comment