SIMBA leo Jumapili imeandika historia katika soka la Tanzania baada ya kukubali na kubariki mfumo wa uwekezaji na kumkubalia Bilionea Mohamed Dewji ‘Mo’ kuwa mwekezaji wa klabu hiyo.
Mo amepita katika mchakato wa uwekezaji ambao ulikuwa unasimamiwa na Kamati Maalumu ya zabuni ya Simba iliyokuwa inaongozwa na Mwenyekiti Jaji Mihayo.
Jaji Mihayo alisema kuwa Mo ndiye mwekezaji pekee aliyejitokeza kuomba zabuni hiyo mara baada ya kutangazwa kwa mchakato huo huku akikidhi vigezo vyote vilivyowekwa.
Jaji Mihayo alieleza kuwa mwekezaji huyo atakuwa akiweka mipango yote ya klabu ikiwemo kusajili wachezaji, kuajiri benchi la ufundi, kutengeneza viwanja vya mazoezi, gym, hosteli ya wachezaji, kuanzisha ‘academy’, Bwawa la kuogelea na Jengo la ofisi za klabu.
“Mfanyabiashara maarufu nchini Mohamed Dewji ‘Mo’ amepita katika mchakato wa awali wa uwekezaji wa klabu ya Simba kwa kukubaliwa kuwekeza Sh 20 bilioni ambapo majadiliano zaidi yatafanyika baada ya mkutano wa leo Jumapili. Mo alikuwa mwombaji pekee aliyetuma maombi katika Kamati yetu na ndiye mshindi wa tenda, ametimiza vigezo vyote.“Hivyo mwekezaji amekidhi vigezo vyote na tumejiridhisha kupitia Kamati Maalumu ya kutathimini Zabuni, lakini pia tunaangalia jinsi gani ataweza kulipa madeni ya klabu ya sasa, kodi za klabu ambazo wanadaiwa na TRA na hatima ya michezo mingine, ” Jaji Mihayo
Jaji Mihayo amesema kuwa mwekezaji pia ameeleza jinsi ya kuwa na vyanzo vya mapato kwa klabu ikiwemo mapato ya getini, kodi za majengo, riba za fedha zitakazokuwa benki, uuzaji wa jezi, kofia na mengineyo.
No comments:
Post a Comment