IMETHIBITIKA kuwa beki Mghana, Asante Kwasi, anayeichezea Lipuli, atavaa uzi wa klabu ya Simba katika mechi zijazo baada ya kusainishwa mkataba wa miaka miwili.
Beki huyo mwenye mabao matano katika Ligi Kuu Bara akiwafunika hata baadhi ya mastraika wa klabu kubwa nchini, alitarajiwa kusainishwa mkataba huo jioni ya jana Jumatatu baada ya kumalizana na mabosi wa klabu hiyo pamoja na wale wa Lipuli.
Kocha Mkuu wa Simba, Joseph Omog, kabla ya kwenda mapumzikoni kwao Cameroon, alipendekeza asajiliwe beki wa kati anayeweza kucheza pia pembeni na kura zikamwangukia Mghana huyo aliyeichezea Mbao msimu uliopita.
Taarifa ambazo Mwanaspoti imezipata mchana wa jana kabla ya kwenda mitamboni, ni kwamba kila kitu kilishamalizwa juu ya beki huyo na mabosi wa Msimbazi walipanga jioni asainishwe mkataba huo wa miaka miwili.
Kiongozi mmoja wa Simba (jina limehifadhiwa) alilidokeza Mwanaspoti kuwa walishaongea na Kwasi kutua Msimbazi hata kabla msimu huu haujaanza ila walikwama njiani, lakini safari hii hawafanyi makosa na kumsajili rasmi.
“Tumeshamalizana kila kitu na Kwasi muda wowote leo (jana) anaingia hapa Dar es Salaam na atakuja ofisini kabla ya jioni kusaini mkataba wa miaka miwili,” alisema bosi huyo aliyekataa jina lake kutajwa gazetini.
Kocha Msaidizi wa Simba, Masudi Djuma, alithibitisha benchi la ufundi kumuidhinidha Kwasi.
No comments:
Post a Comment