SIMBA wameipeleka timu kwa tajiri Mohamed Dewji ‘MO’. Hakuna kitu cha ajabu hapo. Ni kitu cha kawaida kabisa katika mpira wa kisasa. Bahati mbaya tumechelewa. Mchakato kama huu ilibidi ufanyike miaka 25 iliyopita.
Hata hivyo, Waingereza wanasema ‘Better late than never’. Afadhali uchelewe kuliko kutofanya kabisa. Timu hizi za mashabiki au wanachama, ilibidi ziende katika mfumo mpya. Mfumo wa uendeshwaji na kampuni moja au mtu mmoja.
Chelsea inamilikiwa na Roman Abramovich. Manchester United inamilikiwa na familia ya Malcolm Grazer. Arsenal inamilikiwa na Stan Kronke. Maisha ya soka la kisasa ndivyo yalivyo. Timu ikimilikiwa na mkutano wa wanachama haipati ufanisi mzuri. Pamoja na mabadiliko haya, lakini najua kuna watu wa Simba hawajajiandaa kisaikolojia kwa mabadiliko haya. Sio wale wachache wanaopinga tu, bali hata baadhi ya watu waliopiga kura ya kuafiki bado hawajui kitu walichokifanya. Kwanza kabisa, lazima waelewe kuna nguvu kubwa wameipunguza kwa makusudi na kumwamini mtu mmoja aiendeshe timu yao vyema. Hata hivyo, Simba inabakia kuwa klabu ambayo uwanjani itabidi ishindane kama ilivyo kwa klabu nyingine.
Nongwa kubwa inaweza kutokea wakati Simba haifanyi vizuri uwanjani. Hapo ndipo wale ambao hawaungi mkono kilichofanyika wataibuka na kuidai timu yao. Nabashiri pia kuna baadhi ya waliounga mkono nao wataanza kujutia uamuzi wao. Huo utakuwa ujinga. Pia kuna baadhi ya viongozi hawatakwenda katika timu mpya ya uongozi wa MO, hao nao baadaye wanaweza kuwa sehemu ya wapika majungu kama Simba haitafanya vizuri chini ya tajiri MO.
Kuna baadhi ya makomandoo ambao ulaji wao utakuwa umeondoka baada ya MO kuchukua timu kwa sababu ataweka watu wake walio chini ya kampuni yake ambao watakuwa wanaendesha shughuli za kila siku klabuni. Hawa nao watakuwa wapika majungu wazuri tu. Ukweli utabakia pale pale, Simba imeondoka katika mikono yao. Kitu pekee kwa wakati huo ambacho wanaweza kufanya ni kununua hisa za MO au kumlazimisha auze kwa tajiri mwingine. Huu ndio ukweli ambao inabidi waumeze. Hawapotezi haki ya kumtaka MO aiachie klabu yao, lakini hawana haki ya kumlazimisha aiachie timu pindi watakapoona mambo yanakwenda kombo. Haya ndio mabadiliko ambayo wameyakubali kwa roho safi kabisa. Kuanzia hapo natazamia kuona Simba ikibadilisha matajiri zaidi. Siku ambayo MO ataichoka Simba au ataona haimpi faida aliyokusudia bado klabu haiwezi kurudi katika mfumo wa zamani. MO mwenyewe atamtamfuta tajiri mwenzake na kumuuzia hisa zake.
Kitu kizuri zaidi kwa Simba, kama MO akitimiza ahadi zake alizotoa juzi pale ukumbini ni wazi thamani ya Simba itaongezekana na tajiri ajaye anaweza kujikuta akiinunua kwa zaidi ya Sh100 bilioni. Kitu ambacho kinanishangaza mpaka sasa ni kuona jirani zao, Yanga wakiwa kimya kama vile hawaelewi Simba wanafanya kitu sahihi ambacho hawana budi kukiiga. Wanapaswa kuanza mchakato wao mapema. Sio Yanga tu, hata klabu nyingine ambazo zinaendeshwa kwa mfumo wa wanachama inabidi zibadilike, kama vile Coastal Union na African Sports za Tanga ambazo zina hazina ya mashabiki wengi kuliko hata Azam FC. Tupo katika dunia ya ubepari na tunapaswa kuondoa mawazo ya kijamaa.
Kama ambavyo tumebinafsisha viwanda, benki na mashirika ya umma, wakati umefika sasa kuzibinafsisha klabu zetu ambazo zinaendeshwa kama mashirika ya umma ya zamani.
Hakuna namna yoyote ambayo wanachama wanaweza kuzisaidia kwa dhati klabu hizi kwa sababu kila mmoja haioni kama ni mali yake binafsi. Mtu kama Mo ataiona kama mali yake binafsi na atawekeza pesa nyingi kwa sababu anajua itamlipa siku za usoni.
Huu ni mwisho wa kuishi na watu wanaoitwa wafadhili. Ni mwanzo wa kuishi na watu ambao kwa uwazi kabisa watanufaika na hizi timu kuliko kuwa na watu ambao tunataka waingize pesa bila ya wao kunufaika. Kila la kheri Simba, kila la kheri MO.
Hi kasuluwadau
ReplyDeleteNjoo tukuwekee adsense kwenye blog yako
0686855721