Ndugu Mheshimiwa Spika wa Bunge tukufu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mheshimiwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo,
Waheshimiwa Wabunge,
Viongozi wenzangu na Wafanyakazi wote wa SportPesa,
Waandishi wa habari, wageni waalikwa,
Mabibi na Mabwana.
Habari za Mchana,
Nina furaha ya dhati kusimama mbele yenu kama mwakilishi wa kampuni ya SportPesa leo hii katika tukio hili kubwa la kihistoria katika tasnia ya mpira wa miguu nchini la kukabidhi uwanja wa taifa kwa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hakika ni siku ya kukumbukwa sana.
Historia ya marekebisho ya uwanja huu wa taifa inaanza mwezi Juni mwaka huu ambapo kampuni ilikuwa ikijiandaa na ujio mkubwa wa klabu ya Everton nchini.
Wakati tunafikiria kuileta Everton kulikuwa na wataalamu kutoka Uingereza ambao walikuja hapa kuangalia vitu mbalimbali kama vile usalama wa timu zao, malazi kwa maana ya hoteli, usafiri na mwisho wakasema wanataka kuona miundombinu ya kuchezea kwa maana ya uwanja kwasababu na wao wana vigezo vyao hususani kwenye sehemu ya kuchezea, vyumba vya kubadilishia jezi na vyoo ambavyo vilikuwa ni lazima vikidhi viwango vya kimataifa.
Tuliweza kufaulu kwenye hoteli, usalama na usafiri vilevile suala la mizunguko kwasababu unajua Dar es Salaam ni moja ya sehemu zenye foleni, lakini ilipokuja kwenye uwanja hatukufaulu kwasababu uwanja ulionekana haufai
Tulikuwepo wakati wanachimba kuangalia udongo ukoje, nyasi zikoje kama zinaweza kufaa kuchezea mpira, kwetu sisi watanzania zilikuwa zinafaa lakini kwao hawakuona hivyo.
Wakaenda kuangalia miundo mbinu mingine kama vile vyumba vya kubadilishia nguo, vyooni na sehemu nyingine na walichukua sampuli wakaondoka nazo kwenda Uingereza kuangalia lakini kwa kweli tulifeli.
Sasa kilichotokea kwa SportPesa ili kuweza kuileta Everton, ilikuwa ni lazima kutengeneza upya uwanja kwenye sehemu ya kuchezea na vyumbani.
Muda ulikuwa hautoshi na wataalam wakaja kuangalia wanawezaje kuutengeneza uwanja katika hatua ya awali ili kuiwezesha Everton kuja kucheza.
Zikatengenezwa nyasi ambazo zinaweza kuota haraka ili kwa wiki tatu au nne ziwe zimeshakamilika, lakini nyasi hizo zisingeweza kudumu, sana sana zitumike kwa miezi mitatu na baada ya hapo ije awamu ya pili ambayo itengeneze nyasi za kisasa zitakazodumu kwa kipindi kirefu hata miaka kumi ambazo hata gharama yake ni kubwa na ingechukua kipindi kirefu.
SportPesa imetumia gharama kubwa kuweza kutengeneza ile hatua ya kwanza na hii hatua ya pili ambayo imekwangua kila kitu tukaanza upya na pia ukienda kwenye vyumba vya kubadilishia nguo kwasasa ni vya kimataifa kabisa, sote tumekuwa mashahidi katika hilo.
Sababu kubwa ya SportPesa kufanya hizo kazi si tu kwasababu ya Everton inakuja, lakini pia kuweza kutoa mchango wetu kwa taifa la Tanzania ili kuweza kuwa na miundombinu bora zaidi ambayo ina viwango vya kimataifa.
Ukumbuke kuwa Tanzania itaandaa mashindano ya vijana ya mwaka 2019 na uwanja ule utakuja kupimwa ili kuona kama umefuzu viwango vya kimataifa. Na hali ilivyo sasa ni lazima watasema Naam! Na hiyo yote ni kwasababu ya SportPesa.
Mabibi na mabwana!
Nirudie kusema kuwa ni fahari kubwa sana kwetu sisi kama SportPesa na ni heshima pia kuwa sehemu ya marekebisho haya ya uwanja wa taifa na tunaishukuru serikali kupitia Wizara ya habari, Utamaduni Sanaa na Michezo kwa kuonesha ushirikiano wa dhati tangu tunaanza mpaka hapa tulipofikia.
Mwisho kabisa niwatakie kila la kheri waheshimiwa wabunge kwenye michuano hii ya mabunge ya Afrika Mashariki. Sote tunaamini kuwa waheshimiwa watabakiza makombe yote nyumbani wakiwa wanang’aa kwenye uzi wa SportPesa.
Asanteni!
No comments:
Post a Comment