SIMBA KIMYA KIMYA MJINI , YANGA WAPIGA HESABU ZA KUTETEA UBINGWA>>>> - KASULU WADAU BLOG

Breaking

ONLINE

Monday, December 18, 2017

SIMBA KIMYA KIMYA MJINI , YANGA WAPIGA HESABU ZA KUTETEA UBINGWA>>>>

HATIMAYE jeuri ya Yanga juu ya tambo zao za kutetea ubingwa wao wa Ligi Kuu Tanzania Bara na kuwakata ngebe watani wao wa jadi waliopo kileleni kwa ligi hiyo, Simba, imebainika.

Simba kwa sasa ndio wanaoongoza ligi hiyo wakiwa na pointi 23 sawa na Azam waliopo nyuma yao, lakini Wekundu wa Msimbazi hao wakiwa kileleni kutokana na kubebwa na idadi kubwa ya mabao ya kufunga.

Ndani ya mechi kumi na moja kwa timu zote zinazoshiriki Ligi Kuu Bara, Simba wamefunga mabao 23 na kufungwa sita, huku Azam wakiwa wametikisa nyavu za wapinzani wao mara tisa na zao kuguswa mara tatu tu.

Yanga wanaoshika nafasi ya tatu wakiwa na pointi 21, wana mabao 17, huku wakiwa wameruhusu matano, wakati Singida United iliyopo nafasi ya nne ikijikusanyia mabao tisa na kufungwa matano na hivyo kuwa na pointi 20, ikiizidi Mtibwa Sugar kwa pointi mbili, yenyewe ikiwa imecheka na nyavu mara nane na nyavu zake kutikiswa mara tano.

Pamoja na kuongoza ligi hiyo, bado Simba imeonekana kutobweteka na hivyo kuamua kufanya usajili wa kishindo, wakimtwaa beki mahiri wa Lipuli FC, Mghana Asante Kwasi, Antonio Domingos wa Msumbiji na Mzambia Jonas Sukuwaha, ili kuboresha zaidi kikosi chao na hatimaye kutwaa ubingwa wa Bara pamoja na kufanya vema kimataifa.

Kwa upande wao, Yanga wanaotetea ubingwa wao, hawajafanya usajili wowote wa maana zaidi ya kumsajili kinda wa Serengeti Boys, Yohana Mkomola na Fiston Kayembe raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kutokana na kukosa fedha za kuwawezesha kuwanasa nyota waliokuwa wakiwapigia hesabu kama Mohammed Issa ‘Mo Banka’ wa Mtibwa, Mohammed Rashid wa Prisons na wengineo kutoka ndani na nje ya nchi.

Lakini pamoja na hilo, Yanga bado wameonekana kuwa na jeuri ya kutetea ubingwa wao wakidai hawatishwi hata kidogo na Simba pamoja na mbwembwe zao, wala Azam, Singida United na Mtibwa Sugar.

Tumedodosa dodosa sababu za nyodo hizo za Yanga na kubaini mambo mawili, zaidi ikiwa ni morali ya wachezaji wao, wanachama, mashabiki pamoja na viongozi wa klabu hiyo.

Katika hilo, Yanga inaamini kutokana na morali waliyonayo wachezaji wao iliyowawezesha kuwa nyuma ya Simba kwa pointi mbili, hakuna la kuwazuia kuendelea kufanya vema kwenye mechi zijazo za Ligi Kuu Bara, hasa kwa kipindi hiki ambacho wachezaji wao watakuwa wamelipwa mishahara yao yote.

“Kama tuliweza kukabiliana na mbwembwe za Simba wakati tulipokuwa katika wakati mgumu kifedha, wachezaji wakiwa hawajalipwa mishahara kwa miezi mitatu, tutashindwaje kuwang’oa Simba kileleni kwa wakati huu suala la fedha likiwa si tatizo?” alihoji mmoja wa viongozi wa timu hiyo aliyepo katika Kamati ya Mashindano ambaye hata hivyo, hakutaka jina lake kuwekwa hadharani.

Jeuri nyingine ya Yanga ni kitendo cha timu yao kutopanguliwa kwani wachezaji wale wale waliouanza msimu, wataendelea kuunda kikosi cha kwanza na hivyo kuwa na kombinesheni ile ile pamoja na maelewano kuanzia ndani ya uwanja hadi nje.

Kocha Mkuu wa Yanga, George Lwandamina, ameliambia BINGWA kuwa pamoja na kutofanya usajili wa wachezaji nyota kipindi hiki cha dirisha dogo, kwa wale walionao, ana uhakika wa kutwaa ubingwa wa Bara na hata kufanya vema kimataifa.

“Unapokuwa na wachezaji waliokaa pamoja kwa muda mrefu, unakuwa na nafasi kubwa ya kufanya vizuri zaidi, kwani wanakuwa wamezoeana na wakifahamiana uchezaji wao, nadhani hili litatusaidia sana.

“Hata hivyo, nikiri kuwa unaweza kuingiza mchezaji mpya kikosini na timu ikawa nzuri zaidi kutegemea na ubora wa mchezaji husika, ninachoweza kusema ni kwamba bado nina timu bora na wale wachezaji wetu tegemeo waliokuwa majeruhi, wanarejea kuongeza nguvu zaidi katika kikosi chetu, hivyo sina wasiwasi hata kidogo,” alisema.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Hussein Nyika, alisema: “Azma yetu ya kutwaa ubingwa ipo pele pale, hapo hatujasajili wachezaji wengi, hao wawili tuliofanikisha wana uwezo wa kuongeza nguvu katika kikosi chetu na kuwa bora zaidi ya awali.”

Yanga imeitawala Ligi Kuu Bara kwa msimu wa nne sasa ikiibuka kidedea, huku watani wao wa jadi, Simba, wakiishia kunawa na kuiacha vita ya kuwania kombe ikibaki kwa Wanajangwani hao na Azam kwa kipindi chote hicho.

No comments:

Post a Comment